Mke wa zamani wa Nelson Mandela, Winnie amewasili katika hospitali nchini Afrika Kusini, ambako inaaminiwa rais huyo mstaafu anaendelea kupokea matibabu kwa ugonjwa wa homa ya mapafu.
Mtoto wao wa kike Zenani (mandela - Dlamini) pia amerejea nchini Afrika Kusini kutoka Argentina ambako anahudumu kama balozi wa Afrika Kusini, ili awe na babake.
Bwana Mandela, mwenye umri wa miaka 94, alipelekwa hospitalini mapema Jumamosi , ikiwa ni mara ya tatu kulazwa hospitalini mwaka huu.
Kwa mujibu wa duru za urais, Mandela amekuwa akiugua kwa muda mjini Johannesburg baada ya kukumbwa tena na ugonjwa wa mapafu. Msemaji wa serikali Mac Maharaj amesema kuwa maafisa katika hospitali wanataka kudhibiti idadi ya watu wanaozuru hospitali hiyo ili wampunguzie bwana Mandela usumbufu.
Alilazwa hospitalini baada ya hali yake kuwa mbaya zaidi mnamo Jumamosi.
Kwa mujibu wa taarifa za urais, President Jacob Zuma, amerejelea wito wake kwa watu nchini Afrika Kusini kumuombea Madiba wakati huu anapougua.
Lakini mwandishi wetu mjini Pretoria, Karen Allen, anasema kuwa kuna matumaini madogo kuwa Mandela aliyeongoza vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, huenda akapona.
Anasema kuwa wengi walipata matumani baada ya bintiye Mandela Zindzi, kusema kuwa babake yuko salama na kuwa anaendelea kupata nafuu.
Mkewe Mandela Graca Machel, alifutilia mbali, ziara yake mjini London Jumamosi ili kuwa kando ya mumewe.
Mandela alikuwa Rais wa Afrika Kusini kati ya mwaka 1994 hadi 1999.
Alifungwa jela miaka 27 na anaaminika kuwahi kuugua ugonjwa wa mapafu alipokuwa akifanyishwa kazi ngumu katika machimbo ya mawe akiwa jela.
0 comments:
Post a Comment